Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Kwa kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad Mustafa (saw), hafla ya kidini na kitamaduni imefanyika tarehe 2 Septemba 2026 katika Hawza Imam Ridha (as), Ikwiriri, Mkoa wa Pwani, ikihudhuriwa na wanafunzi, walimu, waumini pamoja na Waislamu wa Shia na Sunni.
Katika hafla hiyo, wanafunzi wa Hawza, walimu na waumini kutoka Ikwiriri na maeneo ya jirani wamekusanyika kwa ajili ya kuadhimisha Maulid ya Mtume Muhammad (saw) kupitia programu mbalimbali za kidini na kitamaduni.
Katika sehemu ya hotuba, mzungumzaji ameeleza fadhila, sifa njema na nafasi tukufu ya Mtume Muhammad (saw), huku akiwafahamisha washiriki kuhusu vipengele mbalimbali vya maisha yake yenye nuru na mwenendo wake bora wa kimaadili.
Aidha, sehemu nyingine ya hafla hiyo imeangazia upendo na huruma ya Mtume Muhammad (saw) kwa watoto, ambapo imesisitizwa kuwa ni muhimu kuwapa watoto upendo, kuzingatia mahitaji yao na kuwalea kwa malezi sahihi ili kujenga kizazi chenye maadili mema.
Mzungumzaji pia amesisitiza umuhimu wa kuwalea watoto katika msingi wa kuipenda Qur’ani Tukufu, Mtume Muhammad (saw) na Ahlul-Bayt (as), akieleza kuwa malezi hayo ni miongoni mwa misingi muhimu ya kukuza kizazi chenye ustawi wa kiroho na kimaadili.
Hafla hiyo ni sehemu ya shughuli za kidini, kitamaduni na kielimu zinazofanywa na Hawza Imam Ridha (as) huko Ikwiriri, na imekuwa hatua katika kueneza maarifa ya Kiislamu, kuimarisha uhusiano na jamii ya Waislamu, pamoja na kukuza utamaduni wa kumpenda na kufuata mwenendo wa Mtume Muhammad (saw) na Ahlul-Bayt (as).
Imeandaliwa na: Kitengo cha Mahusiano ya Umma – Uwakilishi wa Jamiat Al-Mustafa (s) Tanzania
Maoni yako